Fatwa

Frequently Asked Questions

Question What is the ruling on taking an interest-based loan due to the economic circumstances associated with the coronavirus (COVID-19) pandemic?

Answer

In the name of Allah, the Most Merciful, the Most Beneficent. All praise belong to Allah, and may prayers and peace be upon Allah’s Messenger, his family, his companions, and those that follow them. Interest-based loans are not permitted unless due to sever necessity. This has been determined by various assembly resolutions, beginning with the Assembly of Islamic Research in 1965, and others over the years. Widespread needs could be included in the necessities that permit what is otherwise impermissible. Apply that ruling to this situation depends on a very accurate description of the conditions. Are we facing a need to secure the necessities of life? Are we facing a need to a protect fundamental wealth and prevent it from decline and collapse? If the situation is such, then the concession permits only what is required while at the same time striving to get rid of it. If the situation is not as such, then taking interest-based loans is prohibited as usual. And Allah the Exalted knows best.

Swali

Je ni halal kipato ninachopata kutokana na uwekezaji katika hati fungani za serikali (Treasury bills or bond) au za mashirika (corporate bond) mfano wa Jasiri Bond ya NMB au kupitia mfuko wa UTT wa hati fungani (Bond Fund).

Jibu

Aina zote za Hati Fungani ulizotaja hapo juu ni makubaliano ya kukopesha inayompa mkopeshaji ziada au riba. Serikali au kampuni zinakopa kwa wananchi hela na kurudisha hela hizo na ziada ambayo Kisharia ni aina moja wapo ya Riba iliyokatazwa.

Hivyo kipato cha ziada kinachotakana na hati hizo sio Halal katika Sheria yetu tukufu ya Kiislam na uwekezaji wake sio Halal.

Tunazishauri mamlaka husika zitumie utaratibu wa Sukuk ambazo kila mwananchi atawekeza na kunufaika na kipato chake bila kufitinishwa na imani ya dini yake. Pia tunawashauri waislam wote wakae mbali na njia hizo za hati fungani ambazo sio halali kwao.

Swali

Je halmashauri au serikali za mitaa, au wizara zinapotoa mikopo ya fedha taslimu kwa watumishi wake kwa ajili ya kununuwa magari, pikipiki, samani na gharama za matengenezo ya magari na pikipiki kwa kumtaka mkopaji kuchangia bima asimilia 1 (protection fund) na kulipa service fee 3% inafaa muislam kuchukuwa mkopo huo?

Jibu

Uislam ni dini inayopenda watu kujiendeleza kiuchumi na kukidhi haja za kimaisha kwa sharti la zingatia kanuni za kimiamala na maadili mema.

Kukopesha ni katika njia za kusaidiana na ni ibadah iliyowekewa kanuni za kisharia. Moja ya kanuni ya msingi ni mkopeshaji asinufaike kutokana na mkopo anaoutoa kutoka kwa mkopeshwaji. Kwa lugha nyingine asidai nyongeza yoyote katika fedha anayokopesha. Sharti la kuweka nyongeza katika mkopo wa fedha taslimu hupelekea kuingia katika aina moja wapo ya miamala ya RIBA. M/Mungu ametangaza vita kwa wanaojihusisha na miamala hiyo. Pili, mkopo huo utolewe kwa madhumuni ya matumizi katika mambo ya maana na kheri. Tatu, mkopo huo uandikwe na pawepo mashahidi juu yake.

Kwa mujibu wa swali ni wazi kuwa mkopo huu ni wa fedha na mtoaji ima atalipa na zaidi (3%) au atakatwa hiyo (3%) katika mkopo anaoomba na kupewa pungufu (97%) na kurejesha kamili (100%). Kufanya hivyo ni kutoza RIBA na ni makosa katika Sharia ya Kiislam hata kama inaitwa service fee au jina jingine lolote. Pili, makato ya bima yaliotajwa hapa yanahitaji ufafanuzi ili kujuwa hukmu yake. Kimsingi, Uislam unao utaratibu wa bima yake inayoitwa Takaful (mashirikiano na kusaidiana) na unazikataa taratibu za bima ya kuuza na kununua (conventional insurance). Hivyo, bima iliyotajwa hapa haipo wazi sana ili kuitolea maelezo sahihi.

Tunaziomba na kuzishauri taasisi zote za serikali kuzingatia kuwa baadhi ya watumishi wake ni Waislam na hela hizi wanazokopesha watumishi zinatokana na baadhi ya wananchi ambao ni Waislam na hivyo wapewe watumishi haki sawa kwa mujibu wa Katiba bila kuwabagua kwa kuweka taratibu za mikopo ambayo inavunja haki yao ya kuabudu na mafundisho mazuri ya dini yao.

Iwapo serikali inataka kupata faida halali au kufidia gharama fulani, Uislam unazo njia na taratibu nzuri za kupata faida halali isiyokuwa riba au njia murua za kugharamia gharama halisi za kukopesha.

Kwa maelezo juu ya taratibu na njia hizo mbadala wa RIBA.

Swali:

Kila baada ya muda fulani mitandao ya simu Tanzania yenye huduma za kuweka na kutuma fedha kama vile Airtel MoneyM-PesaTigoPesa n.k hutuma meseji inayosema “Umepokea Xxx Tsh kutoka kwa (kampuni ya simu) Gawio La Faida” je ni sahihi mimi kutumia hela hii?


Jawabu:

Tumeshuhudia jambo hili miaka ya hivi karibuni mitandao ya simu yenye huduma ya kifedha kugawa “gawio la faida” kwa wale ambao wanahela katika mitandao hiyo.

Tunavyofahamu kwa mujibu wa Sheria za nchi ya Tanzania ni lazima kwa mitandao hiyo ambayo huwa na hela kadhaa za wateja wao, kuziweka hela hizo benki katika akaunti maalum “Trust Accounts” na benki za kawaida hulipa kiwango fulani cha riba kwenye hela hizo.

Hiyo Riba inayopatikana katika akaunti za mitandao ya simu inagawiwa kwa wale wote walioweka hela zao kila baada ya muda kwa mujibu wa Sheria na hesabu zinazofanyika kila mara.

Kwa ufahamu huu, ni wazi kuwa Riba inayolipwa mitandao ya simu na benki za kawaida ni kipato Haramu kwao na kwetu. Wanaiita gawio la faida lakini hiyo aina moja wapo ya Riba! Kosa letu kwao ni kukubali kwetu kuziwacha hela hizo bila dharura ya Kisharia katika mitandao ya simu huku tukijuwa kuwa hela zetu zinazaa Riba ambayo na sie tunagawiwa sehemu yake. Mola anasema; “.. Saidianeni katika mambo mema na Uchamungu na msisaidiane katika kufanya madhambi na uadui…” (Maida: 02).

Kadhalika, M/Mungu ametangaza vita na kuwalaani wanaojihusisha na miamala ya Riba. Hivyo, ni vyema usitumie wewe binafsi gawio hilo la riba na badala yake zipeleke katika huduma za jamii au kumpa masikini.

Tunazishauri kampuni za simu, kufuata njia zinazokidhi matakwa ya Sheria na Shariah.

Kwa ushauri wa kitaalamu juu ya njia mbadala isiyokuwa na riba wanaweza kuwasiliana nasi kupitia namba; +255788329670

Vikoba

Sisi tupo katika kikundi kinaitwa Vikoba. Tunanunua hisa kwa bei tuliyojiwekea kwa mfano elf 40 kila mwezi. Nikiwa na shida, naenda kukopa hela na kurejesha na ziada ya mkopo niliopewa. Baada ya mwaka, kikoba tunakivunja. Ikiwa niliweka elf 40 kila mwezi kwa mwaka ni sawa na 480,000/-. Kikoba kikivunjwa naweza kulipwa 800,000 au zaidi. Ziada hii inatokana na kikoba kukopesha na kutoza ile ziada kwa kila mkopo. Je kama mwanahisa, ziada hii juu ya mtaji nilioweka ni katika Riba au vipi?

Jawabu

Kwa mujibu wa maalezo ya biashara ya kikoba aina hii ni kuwa wanakopesha hela kwa kutoza ziada ambayo kisharia ni Riba al Qardh (riba ya mkopo). Hivyo, ukiwa ni mwanahisa katika biashara ya namna hii ambayo inakopesha kwa njia za riba au kuuza kitu au kufanya biashara haramu, hupelekea uwekezaji huo kuwa haramu.

Hivyo, unatakiwa kuleta toba na haki yako ni zile hela tu ulizoweka ambazo ni 480,000 na zilizobaki unatakiwa usizitumie kwa ajili yako au wategenezi wako. Wape mafukara na masikini.

Kwa upande mwingine, tunawashauri waislam kuanzisha au kuwa wanahisa wa vikoba vya Kiislam ambavyo havikopeshi kwa riba au kufanya biashara haramu katika Sharia. Tunatoa wito kwa waislam katika mitaa yao na misikiti yao kuwa na vikoba vya Kiislam ili kuwekeza kihalali na kuwezeshana kufanya biashara kwa mikopo ya halali.

Ikiwa mnahitaji msaada wa namna ya kuunda vikoba vya Kiislam, wasiliana nasi kwa namba: +255788329670.

Swali

Moja ya benki maarufu nchini ambayo haina huduma za kifedha za Kiislam imetangaza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka familia masikini. Je inafaa kwa Muislam kuomba ufadhili huo?

JAWABU:

Iwapo ufadhili huo hauna tozo ya maombi, hauna sharti la kufungua akaunti na wao au kufanya kazi kwao baada ya masomo au masharti yanayokwenda kinyume na Shari’ah inafaa kuomba ufadhili huo kutoka katika benki hiyo kwa kuwa kinachotolewa kwa muombaji ni fedha ya msaada au fedha kama zawadi ambayo inafika kwake kwa hukmu ya zawadi au msaada kwa kufaulu kwake na uduni wa hali yake.

Inafahamika katika Shariah kuwa moja ya hukumu ya Kisharia kuhusu chumo la haramu mfano wa Riba ni kuwa mali ya riba ni haramu kwa aliyeichuma na njia ya kujitakasa na pato hilo linapofika mikononi ni kutubia na kutoa pato hilo kuwapa mafakiri na wenye haja katika jamii. Hili ni wajibu kulifanya iwe kwa mtu binafsi au taasisi iliyochuma pato la riba. Utoaji huu haumpi thawabu mtowaji.

Mwisho, mfadhiliwa anausiwa atambue kwa yakini kwamba anayempa msaada huo ni Allah s.w.t na sio benki hiyo. Hivyo, haitokuwa sahihi kwa msaada huo kuipenda au kuitangaza au kufanya kazi au kuweka akaunti yake ktk benki hiyo ya Riba.

Angalizo: Baadhi ya wanachuoni wanaona haifai kuomba msaada huo.

Swali

Mimi nina mashamba ya miti (Mikalatusi) kwa ajili ya kuuza baada ya mavuno (miaka 5 to 10) Vile vile nina miti ya mitiki (Teak trees) kwa ajili ya kuuza baada ya mavuno (15yrs). Je nawajibika kutoa zaka na inakuwaje?

Jawabu

Bidhaa za misitu kama vile miti uliyotaja na miti mingine kama bamboo ambayo hupandwa kwa makusudio ya kuuzwa baada ya mavuno huwajibikiwa kutolewa zaka kama mali ya biashara.
Hivyo, ikiwa imefikia thamani ya nisaab ya gramu 85 za dhahabu na kutimiza mwaka mmoja (hawl) utapaswa kulipa zaka ya kiwango cha 2.5% kwa mwaka wa Kiislam au 2.577% kwa mwaka wa miladia.
Nisaab yake itapatikana baada ya kujumlisha thamani ya miti husika hapo ilipofikia na kutoa madeni unayodaiwa. Ikiwa baki / balansi imefikia nisaab iliyotajwa hapo juu, utawajibika kutoa zaka kila mwaka kwa viwango vilivyotajwa hapo juu.
Ikiwa hauna fedha ya kutolea zaka yake kila mwaka, utaweka hesabu ya kila mwaka na kuja kutoa zaka utakapokuja kuvuna, kuuza na kupata fedha za kutolea zaka yake ya miaka yote. Kwa kuwa miti aina hii inayochukuwa muda mrefu hadi kuvunwa na kuuzwa, na iwapo huna uwezo wa kutoa zaka yake kila mwaka, unashauriwa uusie kulipwa deni hili iwapo utafariki kabla ya kulipa mwenyewe ili kuondosha dhima iliyopo mbele yako.
Hatahivyo, kuna rai ya pili ambayo inasema kuwa nisaab ya miti hii itakuwa thamani ya nisaab ya mazao ambayo ni 653 kilogramu za ngano na kutolewa zaka pale itakapovunwa kwa 10% ikiwa umetumia maji ya mvua au 5% ikiwa imetumia maji ya umwagiliaji au 7.5% ikiwa njia zote mbili zimetumika.

Swali

Nilipokea hela kutoka kwa mteja wangu kwa ajili ya kumuuzia mali yangu ya biashara. Hatahivyo, nilifanya makosa katika biashara kwa kutumia hela hizo na kushindwa kumpa bidhaa na pia nikashindwa kurejesha hela zake kutokana na hali kuwa ngumu. Mteja wangu ameshindwa kuvumilia baada ya kuwa muda mrefu umepita na mie japokuwa ninayo dhamira ya kumlipa lakini hali yangu haijawa nzuri kulipa fedha zote. Amenitaka niwe nalipa laki moja kila mwezi na deni lake lipo pale pale mpaka nitakapomlipa nusu ya fedha zake kwa mara moja. Je hizi laki tano ninazotoa ni riba au sio riba?

Jawabu

Ikiwa mauziano hayakufanyika kwa mteja wako kupata bidhaa, fedha zake zilizoko kwako ni deni ambalo ni wajibu wako kulipa kwa kadri utakavyoweza ikiwa hali yako ni ngumu. Mdaiwa kuchelewesha kulipa deni nje ya makubaliano bila sababu ni dhulma na dhulma ni jambo lililoharamishwa katika Uislam.
Ama ikiwa hali yako ngumu kama ulivyoeleza, Mwenyezi Mungu amemuagiza anayedai kufanya subira mpaka hali ya mdaiwa itakapokuwa imeimarika na kuweza kulipa yote au kwa awamu. Ikiwa mdaiwa aliweka dhamana, mdai anayohaki ya kuuza dhamana hiyo ili kurejesha deni lake. Ikiwa hakuna dhamana na mdaiwa yupo katika hali ngumu, atamsubiria. Subira hii iwe kwa ajili ya Allah na Allah atamlipa kwa kusubiri malipo mazuri.
Mdai atakapodai kupewa fedha fulani iwe laki moja au chochote kile kama cha kumpoza na ikawa malipo hayo hayapunguzi deni na ikawa anatumia fedha hizo kama kipato chake, atakuwa amejihusisha na aina moja wapo ya riba ijulikanayo kama riba katika deni (riba duyun). Hivyo, tunamuusia kumcha Allah na kuchukuwa malipo hayo kama sehemu ya malipo ya deni lake na kulipunguza deni hilo kwa kadri anavyopokea fedha hiyo na asiwe anachukuwa fedha hizo na deni lipo palepale.
Kadhalika, mdaiwa tunakuusia uandike wasia juu ya deni hilo ili lilipwe iwapo hutojaaliwa kulipa katika uhai wako.
Mola awafanyie wepesi wenye madeni kuyalipa na wenye kudai kuwa na subira. Ameen.

Swali

Kikundi chetu kina mikopo ya dharura na mikopo ya kawaida ambayo mwanachama anarejesha bila riba (Qardh hasana). Lakini iwapo atachelewa kulipa hutozwa faini ya asilimia fulani kwa kuchelewesha malipo. Je kufanya hivi ni sahihi?

Jawabu

Kuna misimamo miwili juu ya suala la faini ya kuchelewesha marejesho: -
1. Haifai kutoza faini katika mkopo wa fedha au vitu pale ambapo mkopeshwaji anachelewa kulipa. Quran tukufu inahimiza kupewa muda wa ziada bila faini. Kadhalika, imekatazwa kwa mkopeshaji kunufaika katika mkopo wa fedha kwa namna yoyote.
2. Faini inafaa kwa masharti mawili:
a. Mkopeshwaji ataahidi kwa hiari yake kuwa akichelewa kulipa kwa wakati atatoa ziada fulani kwa nia ya sadaka ambayo itapokewa na mkopeshaji kama msimamizi wake.
b. Mkopeshaji akipokea faini hiyo aitoe katika kusaidia jamii na isiwe sehemu ya kipato chake au asinufaike nayo.
Ikiwa imebainika kuwa mkopeshwaji yupo katika hali ngumu na ikabainika kuwa faini hiyo inazidisha ugumu wa hali yake, ni vyema mkopeshaji asidai ulipwaji wake.

Swali

Je inafaa kuwekeza katika kazi za Sanaa kama vile michoro ya Monalisa na picha za Picasso na mfano wake?

Jawabu

Haifai kuwekeza katika sanaa za michoro ya viumbe vyenye roho. Abu Juhaifa amesema kuwa Mtume wa Allah (swallah llahu alayhi wasallam) amekataza thamani (au malipo ya kukunua) damu, thamani inayolipwa (kununua) mbwa, kipato cha kitendo cha umalaya, amemlaani anayepokeya na anayetoa riba, anayechora mwili (tattoes) na anayechorwa, na mchongaji / mchoraji (vyenye roho)(musawwir). (Sahih Bukhari - Hadith Sahih).

Swali

Je Uislam umeweka kikomo cha faida (profit margin) kwa wafanyabiashara?

Jawabu

Uislam haujaweka kikomo cha faida (profit margin) kwa bidhaa za wafanyabiashara. Suala la faida na bei limewachwa kwa wafanyabiashara wenyewe, mazingira ya biashara husika, aina ya bidhaa na aina ya mfanyabiashara husika.
Pamoja na hivyo, Shariah inahimiza maadili mema yazingatiwe kama vile huruma, kiasi, kuepuka ugomvi, upole na ukarimu. Shari'a imeelekeza kujiweka mbali na vitendo haramu kama vile ulaghai, udanganyifu, kughushi, ukiritimba wa soko, ambayo ni madhara kwa jamii na watu binafsi.

Swali
Sisi ni watu ambao tumekuja pamoja na kuwekeza katika kununuwa viwanja na kuviuza kwa watu ambao hutulipa polepole. Fedha tunazopata hazikai mwaka kwa sababu tunanuwa viwanja vingine na kuviuza nakadhalika. Katika hali hii je tunawajibikiwa na kutoa zaka?

Jawabu

Kila mwaka unapomalizika mnapaswa kufanya tathmini ya thamani ya viwanja mnavyomiliki, fedha taslimu na madeni mnayotarajia kulipwa. Iwapo thamani yake zimefikia nisaab ambayo ni thamani ya gramu 85 za dhahabu, mtapaswa kutoa zaka. Hivyo ikiwa thamani ya viwanja na mengineyo ni million 13 au zaidi utapaswa kutoka zaka 2.5% kwa kufautana na mwaka mahesabu wa Kiislam au 2.577% kwa mwaka usio kuwa wa Kiislam.
Na ikiwa hamna fedha wakati wa kutoa zaka, mtapaswa kutoa zaka hiyo haraka iwezekanavyo pale fedha mnapozipata kutoka katika mauzo ya viwanja hivyo mpaka zaka yote ilipwe kikamilifu.
Hivyo hivyo, wale wanaomiliki nyumba (apartments) kwa ajili ya kuziuza wanapaswa kutoa Zaka.

Swali

Je naweza kumpa zakatul Mal mfanyakazi wangu wa ndani au dereva wangu?

Jawabu

Ikiwa mfanyakazi wako ni katika masikini au mafukara au anamadeni na ana watu ambao wanamtegemea na kuhitaji uangalizi wake hakuna ubaya kumpatia Zaka yako.
Hatahivyo, niwakumbushe waajiri kuwa ikiwa umempa mfanyakazi zaka yako usiwe ni mwenye kuisimulia kila wakati mbele yake au kutaja kuhusu zaka uliyompa kila anapokosea kufanya jambo kwa kuwa Allah amekataza kutoa sadaka kwa masimulizi na kusema maneno ya kuudhi.
Kadhalika, zaka utakayo wapa isiwe sehemu ya mshahara wao, wala isiwe kwa ajili ya kumtaka afanye kazi fulani ndio umpe na asipoifanya humpi. Wala haipaswi kuwa zaka hii anapewa mfanyakazi anayefanya kazi vizuri na asiyefanya kazi vizuri akanyimwa. Wala isiwe ndio sababu ya kutokuwapa mshahara mzuri zaidi eti kwa kuwa unawapa Zaka kila mwaka.
Ili kuepuka shubuhati katika jambo hili ni bora zaka yako ukampa mtu mwingine ili aigawe kwa wafanyakazi wako bila ya kuwambia kuwa imetoka kwako na bila ya wewe kuwambia kuwa imetoka kwako.

Swali

Kampuni yetu ya ujenzi wa majengo ya kuuza kwa ajili ya kuishi na kuuza fremu za maduka. Katika kipindi cha ujenzi huwa tunauza ghorofa au apartment au fremu za maduka kabla ya kumalizika ujenzi (Off floor plan). Je kwenye mali na biashara hii ya majengo ambayo tunauza apartment kwa kupokea fedha taslimu ingali bado hatujakamilisha ujenzi tunawajibika kulipa Zaka?

Jawabu

Kimsingi jengo la ghorofa au nyumba ya chini unayojenga kwa nia ya kuiuza na ikachukuwa mwaka au miaka miwili au zaidi katika ujenzi wake, huwa halitolewi zaka. Lakini iwapo una kusudia kuuza apartment zake au fremu zake za maduka na kupokea hela wakati ujenzi unaendelea (off floor plan), utawajibika kutoa zaka katika biashara hiyo.
Utaratibu wa mahesabu kwa ajili ya utoaji zaka yake ni kama ifuatavyo:
1. Nisaab: Thamani ya ujenzi huo iwe imeshafikai 85gram za dhahabu.
2. Hawl: kutimiza miezi kumi na mbili kuanzia siku na mwezi ambao thamani ya ujenzi ilifikia nisaab.
3. Kiwango cha utoaji: utatoa zaka kwa kiwango cha 2.5% kwa kalenda ya kiislam au 2.577% kwa kalenda ya miladia.
4. Hesabu yake: utachukuwa gharama ya jengo au ujenzi mpaka pale ilipofikia ambayo ni milki yenu (bado haijauzwa) utajumlisha na fedha taslimu ulizonazo kisha utatoa madeni (yasiokuwa na riba) unayopaswa kulipa ndani ya miezi 12 ijayo yanayohusiana na ujenzi huo. Baki (balance) ikiwa imevuka nisaab iliyotajwa hapo juu, utatoa zaka kwa viwango vilivyotajwa hapo juu.
Hivyo kila mwaka utafanya tathmini ya thamani ya jengo kwa kiwango cha unachomiliki (ukitoa zile apartment au fremu za duka ulizouza) na kufanya hesabu kama ilivyoelekezwa hapo juu (4).
Kwa ushauri kuhusu masuala ya zaka wasiliana nasi info@abrarconsult.co.ke

Swali

Bwana Ali ameuza mali yake kwa mkopo wa siku 60 wa Othman kwa shilingi milioni moja na Huyu Abeid amempa waraka wa ahadi ya maandishi bwana Ali kumlipa shilingi milioni moja baada ya siku 60. Kabla ya kufika muda wa siku 60 bwana Ali akaamua kwenda kwa Khamis akitaka kumuuzia huo waraka wa ahadi ya kulipwa shilingi milioni moja kwa kumpa punguzo alipwe laki tisa na tisini na tano.
Bwana Khamis anakubali na kununua waraka huko akitegemea ikifika siku 60 atalipwa na Othman shilingi milioni moja na kupata faida ya shilingi elfu tano. Kiufupi shilingi elfu 5000 ni faida kwa Khamis na Gharama au Hasara kwa Ali. Na Othman analipa milioni moja ile ile. Je muamala wa namna Hio ni halali kwa mujibu wa sheria ya dini.

Jawabu

Swali hili lina mambo mawili ya kisharia. La kwanza linahusiana na kuhamisha haki ya kulipwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine (transfer of right). Kwa upande mwingine inaweza kuwa kuhamisha deni lako kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine (- hawalah - transfer of debt).
Jambo la pili kutoka katika swali hili linahusiana na kuuza haki ya kulipwa kwa bei nafuu kuliko kiwango halisi kitakacholipwa kwa mtu wa tatu (third party).
Suala la kwanza, wanachuoni wanakubaliana kuwa inafaa kuhamisha haki ya kulipwa au wajibu wa kulipa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine panapokuwepo na ridhaa ya pande zote tatu. Hata hivyo, deni lililohamishwa na ikawa aliyehamishiwa hakulipa, mdai anayohaki kurudi kwa mdaiwa wa kwanza (ambaye alihamisha deni hilo).
Kuhusu suala la pili, wanachuoni wanakubaliana kuwa haifai kununua waraka huo wa deni kwa fedha chini ya kiwango cha deni halisi. Na hii ni kwa ajili ya kuchunga kuingia katika riba naseeh. Uislam hauruhusu kuuza deni isipokuwa kwa thamani ya deni lenyewe.
Ama ikiwa Bwana Ali baada ya kupewa waraka huo na Othman na ikawa ndani ya siku 60 akamfuata Bwana Othman na kumpa punguzo alipwe laki tisa na tisini na tano kwa sharti la kwamba Othman alipe kwa haraka, kitendo hicho kinakubalika. Ibn Abbas r.a aliulizwa juu ya mtu ambaye anadai ikawa namwambia mdaiwa “lipa deni langu haraka, na mimi nitakupa punguzo”, akasema kuwa hakuna tatizo kufanya hivyo.
Katika benki, muamala wa kuuza waraka wa deni hufahamika kama bill of exchange discounting, ambao haufai ikiwa katika sura ya swali hili lakini zipo njia nyingine ambazo hufuatwa na benki za Kiislam ili kumuwezesha Ali kupata fedha na waraka wake kuwa ni dhamana.